Tanzania na Comoro zakubaliana kuharakisha mazungumzo na taratibu za kurahisisha na kulegeza masharti ya upatikanaji wa visa za usafiri kati ya nchi hizo mbili

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na Rais wa Umoja wa visiwa vya Comoro Dkt.Ikililou Dhoinine muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo mchana Picha na Freddy Maro.Tanzania na Comoro zimekubaliana kuharakisha mazungumzo na taratibu za kurahisisha na kulegeza masharti ya upatikanaji wa visa za usafiri kati ya nchi hizo mbili ili kurahisisha mawasiliano mbali mbali ukiwamo usafiri kati ya nchi hizo mbili.

Nchi hizo pia zimekubaliana kuharakisha majadiliano na taratibu za kufikia mwafaka kuhusu mpaka wa majini baina ya nchi hizo mbili pamoja na nchi jirani ya Mozambique.

Aidha, Comoro imeiomba Serikali ya Tanzania kuisaidia nchi hiyo kupata nishati ya mafuta ya petroli na dizeli ambayo Comoro inasema kuwa imekuwa ina uhaba mkubwa nchini humo kwa sasa.

Makubaliano kuhusu masuala hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Visiwa vya Comoro, Dkt. Ikililou Dhoinine wakati viongozi hao walipokutana jioni ya leo, Alhamisi, Septemba 15, 2011, Ikulu, Dar es Salaam. Mazungumzo hayo ya leo yamehudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal.

Kiongozi huyo wa Comoro yuko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ikiwa ni ziara yake ya kwanza tokea aliposhika madaraka ya kuongoza Visiwa vya Comoro Desemba mwaka jana. Kabla ya kuchaguliwa kwake kuongoza Visiwa vya Comoro, Dkt. Dhoinine alikuwa Makamu wa Rais wa Visiwa hivyo aliyekuwa anashughulikia masuala ya fedha na ni kiongozi wa kwanza wa Visiwa vya Comoro kutokea Kisiwa cha Moheli.

Rais Kikwete amemwambia Rais Dhoinine kuwa hatua zozote za kulegeza masharti ya visa za kusafiria kati ya nchi hizo mbili zitaongeza uhusiano wa damu kati ya wananchi wa nchi hizi mbili.

“Tunahitaji kumaliza taratibu za kulegeza masharti ya visa kwa ajili ya watu wetu ili kuwarahishia usafiri na kuwawezesha kutembeleana kwa nafasi na urahisi zaidi na hivyo kuongeza mahusiano ya damu baina yao,” Rais Kikwete amemwambia Dkt. Dhoinine katika mazungumzo hayo. Ilielezwa kwenye mazungumzo hayo kuwa mazungumzo kuhusu taratibu hizo yamepangwa kukamilika mwezi ujao, Oktoba, 2011.

Mbali ya kumpongeza kufuatia kuchaguliwa kwake kuongoza Visiwa hivyo, Rais Kikwete amemwambia mgeni wake: “Tulikuwa na uhusiano mzuri sana na Rais aliyekutangulia Rais Sambi. Tunakuahidi kiwango hicho hicho cha mashirikiano ama zaidi Mheshimiwa Rais.”

Kuhusu suala la mpaka, Rais Kikwete amemwambia Dkt. Dhoinine: “Tunahitaji vile vile kukamilisha suala hili la mpaka baina yetu- Tanzania, Comoro na Mozambique – katika Bahari ya Hindi. Tunahitaji kuongeza kasi kulimaliza hili nalo.”

Naye Rais Dhoinine amemwambia mwenyeji wake Rais Kikwete kuwa Comoro sasa ni shwari ukiondoa suala la ukosefu wa mafuta ya petroli na dezeli. “Tunalo tatizo kubwa Mheshimiwa Rais na tunaomba kama mnao uwezo mtusaidie.”

Rais Kikwete amemjibu kuwa pamoja na kwamba Serikali ya Tanzania haishiriki tena katika biashara yoyote ikiwamo ya mafuta, lakini itajaribu kuwashawishi wafanyabiashara wa mafuta nchini kuangalia namna ya kusafirisha mafuta hayo kwenda Comoro.

Mapema mchana, Rais Kikwete alimpokea Rais Dhoinine kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam wakati kiongozi huyo wa Comoro alipowasili nchini. Dkt. Dhoinine yuko nchini akiwa njiani kwenda New York, Marekani, kushiriki katika Kikao cha 66 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*

HTML tags are not allowed.