Kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Leo

??
Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Davis Mwamunyange wakiingia Uwanja wa Uhuru kabla ya kuapishwa leo mchana.

??

Rais wa Afrika ya Kusini Mhe. Jacob Zuma akiwasili uwaja wa Uhuru leo kushuhudia kuapishwa kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo.

 

Baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika waliohudhuria sherehe hizo za kuapishwa leo mchana

Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameapishwa leo majira ya saa tano na nusu asubuhi baada ya kushinda matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010.

Rais Kikwete ameapa mbele ya jopo la viongozi wa serikali wakiwemo Jaji Mkuu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Mkuu Kiongozi, Jopo  la Majaji, Wakuu wa Vyombo vya ulinzi, Viongozi Watatu wa Madhehebu ya Dini, Wazee Wawili kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani  na Karani wa Baraza la Mawaziri.
Baada ya kuapishwa, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alikaa kwenye kiti cha jadi na kukabidhiwa Mkuki na Ngao na wazee wa jadi kama ishara ya uongozi na mafanikio mema.
Naye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal aliapishwa mara baada ya Mheshimiwa Rais kumaliza kiapo chake.
Baada ya dua na sala kutoka kwa viongozi wa dini na madhehebu ya dini, Mheshimiwa Rais Kikwete anategemewa kupokea salamu ya Heshima kutoka kwa majeshi ambapo mizinga 21 itapigwa, bendera ya Rais itapandishwa, gwaride litaunda Umbo la Alpha na hatimaye Rais atakagua gwaride hilo. 
Rais Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuhutubia wananchi wa Tanzania kutokea hapa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Sherehe hizi za kuapishwa rasmi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete zimehudhuriwa na marais watano wa nchi za Afrika akiwemo Mhe. Robert Mugabe wa Zimbabwe, Mhe. Mwai Kibaki wa Kenya, Mhe. Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini, Mhe. Rupia Banda wa Zambia na Mhe. Joseph Kabila wa DRC.
Nao Umoja wa Afrika umewakilishwa na Mhe. Jean Ping ambaye ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika.

One comment on “Kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Leo

  1. Ludovick Simon Mwijage on said:

    Ninachukua fursa hii, kumpongeza Mheshimiwa Dr Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kushinda kipindi cha pili, kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*

HTML tags are not allowed.