Bibi wa Shinyanga aongyesha mapenzi kwa Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete

Bibi mmoja mwenye umri wa miaka 81, na mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, amemchangia Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sh. 200 (shilingi mia mbili ) ili kumwezesha kununua fomu ya kuwania tena Urais wa Tanzania endapo ataamua kufanya hivyo.

Bibi huyo, Milembe Ndugulile, mkazi wa Kijiji cha Manyanga, Kata ya Usanda, Wilaya ya Shinyanga Vijiji, kiasi cha kilomita 15 kutoka mjini Shinyanga, ameweka mchango wake huo wa sarafu moja ya sh. 200 katika mchango wa jumla wa wananchi wa Shinyanga kumwunga mkono Mheshimiwa Rais.

Sh. 200 hizo za Bibi Ndugulile zilikuwa miongoni mwa sh. 1, 482,200/= (shilingi milioni moja laki nne elfu themanini na mbili na mia mbili) ambazo alikabidhiwa Mheshimiwa Rais Kikwete na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Hamisi Mgeja katika halfa fupi iliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini Dar es Salaam.

Katika risala iliyosomwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Stepehen Masele kabla ya Mheshimiwa Ngeja kukabidhi fedha hizo, ilielezwa kuwa fedha hizo zilitokana na michango ya hiari ya papo kwa hapo ya wananchi wa Shinyanga wakati wa tafrija ya kuwasimika makamanda wapya wa UVCCM wa mkoa huo iliyofanyika Machi 31, mwaka huu, mjini Shinyanga.

Mheshimiwa Mgeja alimwambia Mheshimiwa Rais Kikwete kuwa Bibi Milembe Ndugulile alikuwa ameelekeza kuwa fedha hizo, sarafi moja ya sh. 200, zilikuwa ni muhimu kufikishwa kwa Mheshimiwa Rais kama mchango wake binafsi kuonyesha furaha yake kwa uongozi bora, mahiri na wa kujali wa Rais Kikwete katika miaka minne iliyopita.

Mheshimiwa Mgeja alimwambia Rais Kikwete: “Bibi Ndugulile ameniagiza nikuambie kuwa sh. 200 ndiyo uwezo wake. Amesema kuwa ni fedha ndogo, lakini ni ishara ya kuonyesha dhamira yake kuwa ataendelea kuunga mkono uongozi wako kutokana na mengi ambayo umeifanyia nchi hii katika miaka minne iliyopita katika kulinda utaifa, kulinda umoja, kulinda mshikamano, amani na utulivu.”

Mheshimiwa Rais Kikwete alimshukuru kwa dhati Bibi Ndugulile akisema: “Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana kwa kuwasilisha mchango wa Bibi Ndugulile. Ni mchango muhimu sana kwangu, ni mchango unaonyesha upendo wa Bibi huyo kwangu na utanisaidia kuifanya hiyo kazi, baada ya uamuzi kuwa umechukuliwa kuhusu suala hili. Ni mchango ambao nauthamini sana kwa dhati ya moyo wangu na namshukuru sana Bibi.”

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

12 Aprili, 2010

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*

HTML tags are not allowed.